Je naweza kubakwa na mtu ninayemjua
Wanawake wengi wanaobakwa humjua mtu anayembaka. Ikiwa mwanamke lazima aendelee kuwasiliana na mbakaji, itakuwa vigumu sana kwa mwanamke huyo kupata afueni/nafuu kutokana na ubakaji na kuwaambia wengine kuhusu jambo hilo.
Ubakaji unaofanywa na mume au mume wa zamani.
Ikiwa sheria au desturi za jadi humfanya mwanamke kama mali ya mume wake, mume anaweza kufikiria yuko na haki ya kufanya tendo la ngono wakati wowote anaotaka, hata kama mwanamke hataki.
Mwanamke anaweza kubakwa na mpenzi wake.
Mpenzi wake anaweza kusema kuwa yuko na haki ya kufanya tendo la ngono kwa madai yakutumia fedha zake kwa mwanamke huyo, kwa sababu wamefanya tendo la ngono hapo awali, kwa sababu amemfanyia mchezo katika hali inayomvutia au kwa sababu mwanamume ameonyesha hiari ya kumuoa. Lakini mwanamume akimlazimisha mwanamke kufanya hivyo, bado ni ubakaji. Mwanamke anaweza kushindwa kuzungumzia aina hiyo ya ubakaji, kwa sababu anaogopa kulaumiwa na wenzake.
Unyanyasaji wa kijinsia.
Mwanamke anaweza kulazimishwa kujamiiana na mfanyakazi mwenzake, msimamizi wake au mkubwa wake kazini ili aendelee kufanya kazi hapo. Mwanamke anaweza kutishiwa kupoteza kazi yake au kupata adhabu nyingine ikiwa yeye ataelezea mtu yeyote.
Unyanyasaji wa kijinsia wa watoto.
Msichana au mvulana anaweza kubakwa na mtu yeyote yule katika familia au mtu mzima. Ikiwa baba, baba wa kambo, mjomba, kaka, binamu, au jamaa yeyote mwingine wa familia atamlazimisha mtoto kufanya ngono, au kumgusa katika hali ya kingono, hii ni ubakaji. Ni muhimu kutambua kwamba watoto wanaweza kuchanganyikiwa au kutokuelewa kinachofanyika haswa ikiwa wanamwamini anayewanyanyasa. Jamaa wengine wa familia huenda wakakosa kujua unyanyasaji huo, wanaweza kukataa kwamba hufanyika, au wanaweza kusema ni kosa la mtoto.
Kamwe si haki kumlaumu aliyebakwa, haswa ikiwa ni mtoto.