Je nitafanya nini ili nizuie maambukizi ya kibofu cha mkojo na figo
Nenda haja ndogo baada ya kushiriki ngono: Wakati wa ngono, viini kutoka kwa sehemu ya uzazi na sehemu ya kutoa choo vinaweza kuingia kwa mrija wa kutoa mkojo. Hii ndio husababisha maambukizi ya kibofu cha mkojo kwa wanawake. Ili kuzuia maambukizi, nenda haja ndogo baada ya kushiriki ngono. Hii huosha mrija wa kupitisha mkojo (lakini haiwezi kuzuia kushika mimba).
Kunywa maji mengi: Viini huingia katika mwili wa binadamu na kusambaa ikiwa hatakunywa maji ya kutosha, haswa ikiwa anafanya kazi katika maeneo yaliyo na joto kali na hutokwa jasho sana. Viini huanza kuzaana kwa kibofu cha mkojo kilicho tupu. Jaribu kunywa glasi 8 au lita 2 za maji kwa siku. Ikiwa unafanya kazi nje kwa jua kali au kwa chumba kilicho na joto jingi, kunywa maji zaidi.
Nenda haja ndogo kila baada ya masaa 3 au 4: Kukosa kwenda haja ndogo huvipatia viini katika njia ya kupitisha mkojo nafasi ya kuzaana na kusababisha maambukizi. Hivyo basi, usikae kwa muda sana bila kwenda haja ndogo (kwa mfano, unapofanya kazi au kusafiri).
Hakikisha kuwa sehemu zako za uzazi ni safi: Viini kutoka kwa sehemu za uzazi - haswa sehemu ya kupitisha choo - vinaweza kuingia kwenye sehemu ya kupitisha mkojo na kusababisha maambukizi. Jaribu kuosha sehemu zako za uzazi kila siku, na ujipanguze kutoka mbele ukienda nyuma baada ya kwenda haja kubwa.
Ukijipanguza na kuleta mbele, unaweza kusambaza viini kutoka kwa sehemu ya kupitisha choo hadi kwa sehemu ya kupitisha mkojo. Ni vyema kuwafundisha wasichana wadogo njia ifaayo kujipanguza, baada ya kwenda haja kubwa. Pia, jaribu kuosha sehemu yake ya uzazi kabla ya kushiriki ngono. Hakikisha kuwa vitambaa na sodo unazotumia wakati wa hedhi ni safi.