Jinsi gani mioto ya kupikia na moshi hudhuru afya yangu
Wanawake wengi hutumia masaa mengi kutayarisha chakula. Jambo hili linahatarisha afya yao kutokana na madhara yanayosababishwa na mioto ya kupikia na moshi.
Mafuta taa na aina zingine za mafuta na gesi zinaweza sababisha milipuko, mioto au kuchomeka.
Wanawake wanaotumia kuni, makaa ya mawe, samadi au mabaki ya mazao huathirika kiafya. Shida za kiafya zinatokea sana kama aina hizi za mioto na gesi za kupikia zinatumika ndani ya nyumba, moshi hautoki nje ya nyumba haraka. Kama aina hii ya mioto ipo na kemikali kama vile madawa ya kuua wadudu au mbolea iliyopo kwa mabaki ya mimea moshi huwa na madhara sana. Uvutaji moshi kutoka kwa mioto ya kupikia husabisha kikohozi sugu, homa, mkamba, kuathirika kwa mapafu na magonjwa ya mapafu. Uvutaji wa moshi unaotokana na makaa ya mawe husababisha saratani ya mapafu, kinywa na koo.
Wanawake waja wazito wanaovuta moshi wa kupikia huhisi kisunzi, kuishiwa na nguvu, kichefuchefu na kuumwa na kichwa. Mwanamke mja mzito huathirika na magonjwa ya mapafu haraka sana kwa sababu mwili wake hauna uwezo kamili wa kujikinga na maambukizo. Moshi unaweza sababisha mtoto asikue haraka inavyotakikana, awe na uzito chini ya kiwango kinachohitajika au azaliwe mapema.
Wanawake wapo hatarini sana kuliko wanaume kwa sababu wanawake hutumia muda mwingi kuvuta hewa iliyochanganyika na moshi. Watoto wadogo wanaotumia muda mwingi kucheza karibu na jiko wapo hatarini ya kupata homa, vikohozi na maambukizi ya mapafu.