Kuna madhara gani nisipomnyonyesha mtoto
Kampuni ambazo hutengeneza maziwa hutaka akina mama wawape watoto wao maziwa haya badala ya kuwanyonyesha, ili kampuni hizi zitengeneze pesa. Utumizi wa chupa au kuwapa watoto maziwa ya kutengenezwa ni hatari. Mamilioni ya watoto ambao hupewa maziwa ya chupa au maziwa ya kutengenezwa huugua utapiamlo, au hufariki.
Maziwa ya kutengenezwa na yale ya mikebe au maziwa ya wanyama hayamkingi mtoto kutokana na magonjwa.
Maziwa haya ya kutengenezwa huweza kusababisha magonjwa na hata kifo. Ikiwa chupa, chuchu au maji yaliyotumika kutengeneza maziwa haya hayakuchemshwa vizuri, mtoto atakunywa viini na kuanza kuharisha.
Watoto wachanga wanaponyonyeshwa matiti, hutumia ulimi kwa kunyonya. NI tofauti sana jinsi vile mtoto anafanya anaponyonya kutoka kwa chupa. Anaponyonya chupa, mtoto anaweza kusahau kunyonya matiti. Ikiwa mtoto hatanyonya matiti sawasawa, maziwa ya mama yatapungua, na mtoto ataacha kunyonya matiti kabisa.
Maziwa ya chupa yako na gharama kubwa mno. Kwa mtoto mmoja, familia itahitaji kilo 40 za maziwa ya kutengenezwa katika mwaka wa kwanza. Ununuzi wa maziwa hayo kwa siku moja, inatosha kununua chakula kwa familia yako kwa wiki nzima - au hata mwezi. Wazazi wengine hufanya maziwa haya yatumike kwa muda kwa kuchanganya maziwa kidogo na maji mengi. Hii husababisha mtoto kuwa na utapiamlo, kukua polepole na kugonjeka kila mara.
MUHIMU: Mwanamke anayeugua virusi vya Ukimwi anapaswa kufanya uamuzi kuhusu njia salama ya kumnyonyesha mtoto wake. Ikiwa unavyo virusi hivyo, zungumza na mhudumu wa afya kuhusu jambo hilo.