Kwa nini mwanamume humuumiza mwanamke
Mwanamume hutoa vijisababu kadhaa vya kumdhulumu mwanamke - kwamba alikuwa mlevi, alipoteza udhibiti au, mwanamke 'alihitaji kudhulumiwa'. Lakini, mwanamume huamua kumdhulumu mwanamke kwa sababu ni njia ya kupata anachohitaji au kile ambacho anafikiria ni chake.
Mwanamume anapoona kuwa hana udhibiti juu ya maisha yake, anaweza kutumia vurugu ili aweze kudhibiti maisha ya mtu mwingine. Ni jambo la kawaida kwa mtu kutaka kudhibiti maisha yake mwenyewe, lakini sio haki kujaribu kudhibiti maisha ya mtu mwingine, haswa kwa kutumia vurugu.
Hizi hapa ni baadhi ya sababu ambazo wanaume hutumia kuwadhuluma wanawake:
Vurugu huleta matokeo: Humpa mwanamume suluhu ya haraka ya kumaliza mzozo bila ya kuzungumzia mambo na kupata suluhu kamili. Huenda mwanamume akaona kuwa vurugu ni jambo la kufurahisha, na kuwa na nguvu nyingi baadaye. Huenda akataka kuhisi hivyo tena baadaye. Ikiwa mwanamume atatumia vurugu, yeye 'hushinda' na kufanya mambo atakavyo. Huenda muathiriwa akampa nafasi tena wakati mwingine ili kuzuia kuumizwa. Hii humpa mwanamume nguvu zaidi. Husiano zilizo na vurugu hufanyika wakati mtu mmoja yuko na mamlaka zaidi juu ya mwingine.
Mwanamume yuko na dhana potovu kuhusu maana ya kuwa mwanamume. Ikiwa mwanamume anaamini kuwa, kuwa mwanamume inamaanisha kudhibiti kile ambacho mwanamke anafanya, ataona kuwa ni VYEMA kumdhulumu. Wanaume wengine hufikiria kuwa wako na 'haki' kwa mambo fulani - kuwa na mke 'mzuri', watoto wavulana, kufanya uamuzi katika familia - kwa sababu tu wao ni wanaume. Husiano zilizo na vurugu hupatikana pale ambapo mtu mmoja yuko na mamlaka zaidi kushinda mwingine.
Mwanamume huhisi kuwa mwanamke ni mali yake, au anamhitaji. Ikiwa mwanamke 'yuko na nguvu', mwanamume huhisi kuwa labda atampoteza, au hamhitaji. Atafanya awezalo kuhakikisha kuwa mke wake anamtegemea kwa vyovyote vile. Ikiwa wanaume wataendelea kufikiria kuwa wanawake na wasichana ni mali yao - kitu wanachomiliki - huenda wakahisi kuwa wako na uhuru wa kuwatendea wapendalo.
Hana njia nyingine ya kuishi Ikiwa mwanamume amemuona babake au watu wengine maishani mwake wakitumia vurugu wakati mambo yalikuwa magumu maishani, basi huenda hakujifunza njia nyingine ya kuishi.
Sababu hizi zinaweza kuelezea kwa nini mwanamume humdhulumu mkewe, lakini hazimpi ruhusa ya kufanya hivyo.